Na WAMJW-DODOMA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amesema Serikali imejipanga kutoa elimu ili kufikia kiwango cha kuchanja Wananchi 80,000 mpaka 100,000 kwa siku kupitia “Mpango shirikishi na harakishi wa chanjo ya UVIKO-19” awamu ya pili.

Amesema hayo jana alipokutana na Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na Waratibu wa Chanjo lengo kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kuchanja ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19.

“Serikali imelenga kuchanja Wananchi kati ya 80,000 mpaka 100,000 kwa siku, hilo ndio lengo letu kubwa, kwahiyo hawa wanaokuwa Halmashauri ndio wanakuwa karibu na Wananchi ndio maana tumewaita leo ili tupeane miongozo na maelekezo ya kwenda kuhakikisha hilo linatimia “Amesema.

Amesema, Serikali imeshazindua mpango wa pili wa kuhamasisha Wananchi kuchanja unaoitwa “Mpango harakishi na Shirikishi wa pili wa kuhamasisha Wananchi kuchanja dhidi ya UVIKO-19 “wenye lengo la kuchanja Wananchi kwa kiwango kikubwa zaidi ili kuwakinga dhidi ya UVIKO-19.

Aidha, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na Waratibu wa Chanjo kusimamia vizuri zoezi zima la utoaji Elimu kwa jamii ili wananchi wafanye maamuzi sahihi kwa hiari yao kwa kupata Chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Hata hivyo, amesema katika mpango huu wa pili, Serikali imelenga kuhakikisha kuwa,  elimu ya mapambano dhidi ya UVIKO-19 ifike mbali zaidi, hasa kwenye kiwango cha jamii yenyewe kupitia vikundi vyao kuelimishana na kuhamasishana ili kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19.

“Kwenye hii awamu ya pili ya huu mpango tunaenda kwenye jamii, kwa maana ya kwamba tunaenda kushirikisha wana jamii wenyewe katika kuhamasishana, sio kila maelezo lazima yatoke huku juu, tunataka wanakijiji wanamitaa wahamasishane wenyewe kwenda kuchanja. “Amesema Prof. Makubi.

Katika kikao hicho kwa pamoja wamedhamiria kusimamia vizuri matumizi ya fedha zilizotolewa na IMF katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 ikiwemo ujenzi wa Miradi ya ujenzi wa ICU, EMD, miradi ya X-ray,  miradi ya magari ya kubebea wagonjwa, pamoja na kujenga nyumba za watumishi kwenye ngazi ya Halmashauri.

Pia, Prof. Makubi ameelekeza wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kabla ya mwezi Juni 2022 ili kuongeza ufanisi na tija katika utoaji huduma kwa wananchi.

Mbali na hayo Prof. Makubi amewapongeza viongozi wa afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri kwa jitihada walizofanya katika awamu ya kwanza ya Kampeni shirikishi na harakishi ya chanjo ya UVIKO-19, kwa kuhamasisha Wananchi na kupata Chanjo ya UVIKO-19.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa, katika Mkutano huo wamepata nafasi ya kujadili namna mpango wa kwanza ulivyofanikiwa kumaliza takribani Chanjo 1,000,000, changamoto zake na mafanikio ili kujipanga katika mpango wa pili ili wananchi wachanje zaidi na kujikinga dhidi ya UVIKO-19.

Kibali chatolewa kukamatwa kwa aliyekuwa Rais
Mugalu: Nitarudi nikiwa imara