Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa – TAKUKURU, Mkoa wa Katavi imefanya chambuzi nne za mfumo kwenye Halmashauri za Mpanda, Nsimbo, Mlele na Tanganyika kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Stuart Kiondo amewaambia Wanahabari kuwa katika chambuzi hizo, wamekutana na njia mbili tofauti za ukusanyaji kodi.
Amesema wamebaini uwepo wa njia mbili tofauti za ukusanyaji wa kodi ya zuio katika Halmashauri badala ya mfumo mmoja wa ukusanyaji, Mamlaka ya Mapato kukosa uwezo wa kutambua kiasi cha kodi ya zuio inachopaswa kukusanya.
Aidha, Kiondo amesema pia wamebaini uwepo wa baadhi ya wakusanyaji wa kodi ya zuio kutokuwa na weledi wa kutosha juu ya matumizi ya TEHAMA na mifumo, huku baadhi ya walipwaji kutowasilisha stakabadhi za mashine au kuwasilisha kwa kuchelewa.