Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewakaribisha wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) kuwasilisha ushahidi wao kuhusu tuhuma za rushwa kwa madiwani waliokihama chama hicho hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola amesema kuwa ofisi hiyo inawasubiri wabunge hao kuwasilisha ushahidi wao ili waufanyie kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Bado hawajatuletea ushahidi wowote lakini tunasubiri watuletee. Hakuna shida, maadam wamesema hivyo, tunawakaribisha,” Mlowola anakaririwa na Mwananchi.
Nassari na Lema walieleza kuwa wanao ushahidi wa picha na video kuwa madiwani wa Arusha ambao walihama chama hicho hivi karibuni na kujiunga na CCM, waliotangazwa wakati wa tukio la Rais John Magufuli kutunuku kamisheni kwa maafisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) mkoani humo walipewa rushwa.
Hata hivyo, Madiwani hao walikana tuhuma za Nassari na Lema na kusisitiza kuwa walikihama chama hicho kutokana na kuvutiwa na utendaji wa Rais Magufuli. Waliwataka wabunge hao kuweka hadharani ushahidi walionao.