Viongozi wa Taliban wamewasihi watu kuondoka uwanja wa ndege wa Kabul baada ya watu 12 kuuawa kwa kupigwa risasi.
Afisa wa Taliban, ambaye amezungumza na shirika la habari la Reuters bila kutaja jina, amesema vifo hivyo vimesababishwa na risasi au kukanyagana, huku mashahidi wameripoti wataliban wenye silaha wamekuwa wakizuia watu, pamoja na wale walio na hati, kuingia ndani ya kiwanja hicho.
Aidha Afisa huyo wa Taliban amewataka Raia wa Afghanistan waliopo katika uwanja wa ndege kurudi nyumbani ikiwa hawana haki ya kusafiri kisheria kutoka Taifa hilo.
“Hatutaki kuumiza mtu yeyote katika uwanja wa ndege.” Amesema Afisa wa Taliban, ambaye amekataa kutambuliwa.
Uwanja wa ndege wa Kabul unabaki chini ya udhibiti wa Marekani lakini barabara zinazozunguka zinalindwa na Taliban.
Hatua hii imejiri baada ya raia hao kutaka kukimbia kutoka nchini humo ili kuepuka utawala wa Taliban ambao waliutwaa mji huo siku ya jumapili (Agosti 15).