Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, ameagiza Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za kinidhamu kuwachukulia hatua Wakuu wa vitengo vya Ukaguzi wa ndani wa Halmashauri 54.
Waziri Ummy amesema Wakuu hao hawakukagua hesabu za mwisho kabla ya kuziwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jambo ambalo ni ukiukwaji wa Kanuni za Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, ametaka wataalamu wenye CPA walioko kwenye Halmashauri zenye hati mbaya na hati zenye mashaka wabainishwe na wafikishwe katika Bodi ya Wakaguzi (NBAA) ili wachukuliwe hatua.
Waziri Ummy ametoa maagizo hayo leo akiwa jijini Dodoma alipokuwa akizungumza kuhusu Ripoti ya CAG kwa TAMISEMI.