Baada ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC, kusema litawachukulia hatua ikiwemo kutoza faini hadi Shilingi 5,000,000 kwa Madereva na Abiria watakaojisaidia kwenye maeneo yasiyo rasmi mwezi mmoja baada ya kutolewa kwa elimu, baadhi ya wadau wameibuka na kudai NEMC inapaswa kulifanyia tathmini upya suala hilo kabla ya kuanza kwa utekelezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka alitoa tamko hilo jana Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam huku akiwaomba Halmashauri na Wajasiriamali kutumia changamoto hiyo kama fursa ya ujenzi wa vyoo, ili kuepuka uchafuzi wa mazingira, ambapo wadau hao wanasema kuna mambo mengi ya kuyafanyia kazi kabla ya kutoa tamko hilo ikiwemo kuangalia gharama zinazotozwa katika maeneo rasmi yanayotoa huduma za kijamii wakati wa safari.
Wamesema, “NEMC wajipange kwanza wajiridhishe wapite zile sehemu zilizopo zinazohudumu waone uhalisia, pia waangalie hali ya kijiografia, gharama kubwa wanazotoza katika maeneo rasmi ya huduma za kijamii halafu ndio waje na tamko jipya, maana hali ilivyo na wanachokisema ni kama wao hawaishi ndani ya hii nchi kuna shida kwa wafanyabiashara wetu na pia kuna maeneo unasafiri unapita mapori na mapori hakuna mji,” walisema Wananchi hao kwa nyakati tofauti.
Mkurugenzi wa NEMC katika tangazo lake alisema, “tutatoa hii elimu kwa muda wa mwezi mmoja na baada ya mwezi mmoja tutaanza kuchukua hatua tutakapokuta kwamba kuna basi lipo porini Watu wanachimba dawa tutatoa motisha kwa yule ambaye atakuwa anatutumia picha,” kauli ambayo imepikelewa kwa hisia tofauti.