Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania TAMWA kushirikiana na WILDAF pamoja na Global Peace Foundation GPF wameiomba Tume ya Uchaguzi (NEC), kuendelea kuhimiza uchaguzi huru wa haki na usawa na kutengeneza mazingira sawa ya ushindani kwa wagomea wote.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano agosti 12 mwaka huu mkurugenzi mtendaji wa TAMWA Rose Reuben, amesema kati ya wagombea 16 waliochukua fomu za kugombea nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kati yao wanawake ni wawili.
Amesema wametoa mapendekezo kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa.
Ameongoza kuwa TAMWA, WILDAF na GPF chini ya ufadhili wa mfuko wa Maendeleo Wa Wanawake Afrika (AWDF) kupitia mradi wa WANAWAKE SASA wamebaini bado kuna changamoto zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa, baada ya kuendesha midahalo mbalimbali.
“Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi , hukutana na changamoto ya lugha dhalilisha wakati wa kampeni na hata wakati utendaji wao wa kazi ili kuwakatisha tamaa na kuwarusdisha nyuma”
“Kama tunataka uchaguzi huru na haki, na wa kidemokrasia ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha za udhalilishaji dhidi ya wanawake” . Amesema Rose.
Katika hatua nyingine mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, ametoa rai kwa wanawake kukataa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono.