Katika kuelekea kwenye Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 8 Duniani kote, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA, ZNZ, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar – ZAZELA, na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba – PEGAO, kupitia mradi wa kuinua Wanawake na Uongozi, wametangaza Tuzo Maalum ya Uandishi wa Habari za Takwimu za Wanawake na Uongozi.
Tuzo hizo, ni muendelezo wa shughuli zinazofanywa na mradi wa kuinua Wanawake na Uongozi kufikia 50/50 katika ngazi zote kupitia tasnia ya Habari, kwa kuwashajiisha Waandishi wa Habari kwa kuhusisha kazi zilizotolewa kwa aina nne ambazo ni Uandishi wa habari za Makala katika magazeti, Redio, Televisheni, Makala katika Mitandao ya Kijamii.
Kazi hizo za Waandishi zimetakiwa kuwasilishwa katika ofisi ya Chama cha ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) Tunguu karibu na IPA na kwa upande wa Pemba kazi katika ofisi ya TAMWA Chake chake Pemba, ikiwa ni mara ya tatu kufanyika tunzo ya aina hiyo ambapo kwa mwaka jana jumla ya Waandishi 10 walishinda tuzo za umahiri kwa upande wa Magazeti na Mitandao ya Jamii.
Aidha, Waandishi wa Habari twametakiwa kufahamu kuwa kazi hiyo ni ya kuisaidia jamii, hivyo ni muhimu kutumia kalamu zao na vipaza sauti katika kuuelimisha na kuibua kero na sauti za wasio na sauti, huku TAMWA ikitoa wito kwa Waandishi na Wahariri, kuimarisha kada hiyo kwa kufuata kwa vitendo maadili ya Habari na Dawati la Uhariri kuwasaidia Waandishi katika utekelezaji wa majukumu yao.