Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limegoma kukata umeme katika nyumba zilizoko maeneo la Kimara na Kiluvya jijini Dar es Salaam ambazo zilipaswa kubomolewa kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.
Mratibu wa zoezi la bomoabomoa katika eneo hilo, Ephrahim Kinyafu alisema kuwa Tanroads walifika katika eneo hilo tangu majira ya saa nne asubuhi wakiwasubiri Tanesco bila mafanikio.
Kinyafu alieleza kuwa baada ya kuwasiliana na meneja wa Tanesco Kimara, Christopher Nguma alimwambia kuwa hawawezi kuwakatia umeme wateja wao bila kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuwapa notisi ya saa 48.
Aidha, Kinyafu alisema kuwa meneja huyo aliongeza kuwa wamebaini Tanroads bado hawajajipanga vizuri kutekeleza zoezi hilo.
“[Meneja Nguma] aliniambia kuwa ‘Tanroads hawajajipanga, hawawezi kuja kukata umeme leo halafu waje kubomoa nyumba baada ya miezi miwili’,” Kinyafu anakaririwa na Mwananchi.
- NEC yaitahadharisha CUF, yajibu mapigo kuhusu tuhuma
- Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi aliyepotea apatikana akiwa amefariki
Aliongeza kuwa Tanesco waligoma kukata umeme kwakuwa walibaini suala la bomoabomoa katika eneo hilo bado liko mahakamani hivyo walitaka kukamilisha taratibu za mahakama kwanza.
Kwa upande wa meneja huyo wa Tanesco Kimara, Nguma aliwataka waandishi wa habari kuwatafuta Tanroads akieleza kuwa wanayo taarifa kamili ya kinachoendelea kati yao.