Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa mtu yeyote atakayebainika kuhujumu miundombinu ya njia kuu ya umeme wa 400 KV unaoanzia Singida kupitia Manyara hadi Namanga mkoani Arusha kwenda nchini Kenya.
Onyo hilo limetolewa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na TANESCO wenye lengo la kutoa elimu kwa wananchi ya kulinda miundombinu hiyo baada ya kujitokeza kwa baadhi ya watu wasio waaminifu wa Kijiji cha Sagara na maeneo nengine wilayani Singida kudaiwa kuanza kuiba vyuma vya nguzo za umeme wa mradi huo.
Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Singida, Davis Mkwiche amesema inasikitisha sana kuona mradi huo mkubwa unaotekelezwa na Serikali kwa fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi ukianza kuhujumiwa na watu wachache kwa kuharibu miundombinu mbinu yake.
“Njia ya mradi huu hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za ujenzi na kama mambo yatakwenda vizuri miezi miwili ijayo itakabidhiwa kutoka kwa mkandarasi kuja kwetu lakini tukiwa katika hatua hizi za mwisho imebainika baadhi ya watu wachache wenye nia hovu wameanza kufanya vitendo vya hujuma kwenye njia ya kusafirisha umeme,” Amesema Mkwiche.
Naye Mkaguzi wa Polisi Ninga Gewe amesema kwa mujibu wa mwenendo wa makosa ya jinai Tanzania kuanzia kifungu cha 14 hadi 16 kinamruhusu raia au mwananchi mzalendo kumkamata mhalifu bila kumpiga na kumpeleka ofisi ya mtendaji wa kijiji au kituo cha polisi lakini awe ametenda kosa husika na siyo kwa kumuonea, hivyo wamewahasa wananchi kulindana na kuulinda mradi huo.