Chama cha wauguzi Tanzania (TANNA) kimesema kuwa mgogoro uliosambaa kwenye video uliowahusisha wauguzi wawili wa zahanari ya Ishihimulwa iliyopo wilayani Uyui mkoani Tabora, Rose Shirima na James Getogo Chuchu ulikuwa mgogoro binafsi huku wakieleza kuwa alichokuwa anakisimamia muuguzi huyo kilikuwa sahihi.
Hivi karibuni wauguzi hao Rose Shirima (Muuguzi Mkunga) na James Getogo Chuchu (Mtekenolojia wa maabara) video yao ilisambaa wakizozana kuhusu matumizi ya vitendanishi katika kituo hicho huku wakitoleana Lugha zisizo na staha.
“Chama kimebaini uwepo migogoro binafsi ya muda mrefu (personal conflict) baina ya hao watumishi wawili na hata hivyo kabla ya kuanza kurekodi video kulikuwepo na lugha za matusi kutoka kwa mtekinologia wa maabara kwenda kwa Muuguzi hali iliyofanya Muuguzi huyo kugadhabika na kujikuta akimjibu kwa lugha isiyo na staha mtekinolojia huyo bila ya kufahamu kuwa anarekodiwa. Kama chama tunakemea na kulaani kitendo hiki”.
Chama hicho pia kimeeleza kuwa hakuna matumizi ya vitendanishi vilivyoisha muda katika kituo hicho kama ilivyotafsiriwa katika video hiyo ila vitendanishi vilivyopo vinakaribia kuisha muda wake yaani bado vina miezi mitatu mbele mpaka tarehe 14/04/2023 hivyo alichokuwa anasimamia muuguzi kilikuwa sahihi kwa kufuata utaratibu wa mfumo wa udhibiti bidhaa (Stock control system using FIFO and FEFO principles) na alikuwa anasimamia maamuzi ya kikao chao cha ndani.