Serikali nchini, imesema kwa sasa suala la upandaji miti linapaswa kuwa la lazima na kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafikia lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kama ilivyopangwa.

Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wakati akiongoza zoezi la upandaji miti Ihumwa na Msalato Jijini Dodoma hii leo Januari 12, 2023 katika maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema, Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanapaswa kutumika kama chachu ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kurekebisha yale yote yaliofanyika katika kuharibu mazingira.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mdodoma kandokando ya barabara ya Dodoma – Morogoro Ihumwa Jijini Dodoma wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kusheherekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar hii leo Januari 12, 2023.

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti pamoja na kuzisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira. Pia amezitaka taasisi za serikali kupanda miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inaishi.

Dkt. Mpango pia ametoa wito kwa Waandishi wa Habari hapa nchini kutoa kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla. Amesema ni muhimu kwa waandishi wa Habari kutoa habari za mifano ya wale walioweza kutunza mazingira ili wawe hamasa kwa watanzania wengine.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema tayari mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira imeanza kutekelezwa ikiwemo kugawa maeneo yaliopandwa miti kwa taasisi za serikali na binafsi ili waweze kusimamia na kuhakikisha miti hiyo inaishi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule za msingi Ihumwa  mara baada ya kumaliza zozezi la upandaji miti kandokando ya barabara ya Dodoma – Morogoro eneo la Ihumwa Jijini Dodoma.

Naye, mdau wa Mazingira na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda ametoa wito kwa wananchi kuzingatia utaratibu wakati wa upandaji wa miti ikiwemo kuandaa mazingira ya upandaji na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kufahamu aina ya mti na mahali unapopaswa kupandwa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema upandaji miti katika vyanzo vya maji umepewa kipaumbele mkoani Dodoma kwa kuanza na Bonde la Mzakwe ambalo limekua na changamoto ya ukuaji wa miti.

Habari Picha: Buriani Mama Sabina Lumwe
TANNA: Muuguzi Tabora alikuwa sahihi