Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amekutana na kufanya mazungumzo kwa mara ya kwanza na Wamiliki wa gazeti la Tanzania Daima ambalo limezuiliwa leseni yao ya uchapishaji tangu Juni 24, 2020.
Mazungumzo hayo yamefanyika Jijini Dodoma, Ofisi za Wizara ya Habari kwa Waziri Bashungwa kukutana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Tanzania Daima, Gerva Lyenda.
Awali katika mazungumzo hayo, Lyenda aliwasilisha ombi na kwa majadiliano zaidi ya kuiomba Serikali kama itaweza kuwapa leseni ya kuanza kazi ya kuchapisha tena gazeti la Tanzania Daima.
“Gazeti limeajiri watu 90 na wanahangaika kwa kukosa leseni tumejifunza na hatutorudia makosa” amesema Lyenda katika mazungumzo hayo na Waziri Bashungwa huku akishukuru kwa fursa hiyo kwani zaidi ya miezi Nane hawajafanya kazi yoyote.
“Asante kwa kutusikiliza hii ni fursa kubwa kwetu, maana miezi zaidi ya nane ni mingi sana na hatujafanya kazi yoyote,” ameeleza Lyenda.
Kwa upande wake, Waziri Bashungwa amewapa wito wa kuheshimu Tasnia ya habari kwa kuwa wote tunajenga nchi moja.
“Watanzania wa sasa wameamka, wanajua lipi ni baya na lipi ni zuri sasa kama unatoa habari zakupotosha tu utakuwa unawakosea haki yao ya kuhabarishwa” amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa wadau wa tasnia ya habari kuunga mkono dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona haki ya uhuru wa habari inaendana na wajibu na uzingatiaji sheria, kanuni na misingi ya taaluma ya habari.
Gazeti la Tanzania lilifutiwa leseni ya uchapishaji tangu Juni 24, 2020 na Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo, ikiwa ni baada ya kulionya gazeti hilo mara kadhaa huku gazeti lenyewe lililazimika kuomba radhi.
Mazungumzo hayo yanafuatia wito wa Waziiri Bashungwa kuwaomba wadau wa tasnia ya habari wakiwemo wamiliki wa magazeti yaliyofungiwa kwenda kufanya naye mazungumzo.