Tanzania huenda ikapata bahati ya kuwakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa barani Afrika msimu ujao 2020/21, kufuatia tetesi za kujitoa kwa mataifa ya Libya, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini kwenye michuano ya Klabu bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Tanzania inafikiriwa kuwa kwenye bahati ya kupata wawakilishi wanne kutokana na viwango vya Shirikisho la soka barani Afrika CAF kulinganisha na nchi nyingine.
Kwa mujibu wa viwango vya CAF, Libya ambayo haijafanya mashindano ya Ligi tangu mwaka jana kutokana na suala la usalama, ipo nafasi ya 12 ikiwa na alama 16.5 na kufuatiwa na Tanzania katika nafasi ya 13 kwa kuwa na pointi 14.
Kwa utaratibu wa kawaida, nchi ambayo haina mashindano ya ligi, inapoteza nafasi ya ushiriki katika mashindano ya CAF na hivyo kutoa nafasi kubwa kwa Tanzania kuwakilishwa na timu zaidi ya mbili msimu ujao.
Mbali ya uwezekano wa kufaidika na nafasi ya Libya, pia hatua ya kujitoa kwa nchi za Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, inatoa nafasi kubwa kwa Tanzania kuongezewa nafasi katika mashindano hayo.
Tayari CAF imetangaza majina ya timu ambazo zitashiriki katika ligi ya mabingwa kwa upande wa nchi zenye nafasi nne na Libya haipo katika orodha hiyo.
Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alikataa kuzungumzia suala hilo huku Katibu Mkuu wake, Kidao Wilfred amesema wameona kwenye mitandao taarifa hizo na wanasubiri taarifa kama ni kuna ukweli.
Sisi tumeona kama wewe, tunasubiri taarifa kama.kuna ukweli wa suala hilo,” alisema Kidao.
Afisa mtendaji mkuu (C.E.O) wa klabu ya Azam, Abdulkarim Amini alisema kuwa na wao wamesikia taarifa hizo na wanafanya juhudi kumaliza nafasi ya pili.