Baada ya kuiwezesha Dodoma FC kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu 2019/20, kwa kuifunga Gwambia FC bao moja kwa sifuri mwishoni mwa juma lililopita, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mbwana Makata, juma hili anatarajiwa kukabidhi ripoti ya kiufundi kwa uongozi wa klabu hiyo.

Makata atafanya hivyo kwa misingi kuwasilisha mapendekezo ya usajili wa ambao utafanya maboresho madogo ili kukiimarisha kikosi chake, ambacho msimu ujao 2020/21 itashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dodoma FC imepanda Ligi Kuu baada ya kumaliza msimu ikiwa vinara wa Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza kwa kujikusanyia alama 51, huku Gwambia FC wakiwa vinara wa msimamo wa kundi B kwa kufikisha alama 47 na kupanda daraja.

Kocha Makata alisema hatofanya maboresha makubwa katika kikosi chake na atabaki na asilimia kubwa ya wachezaji waliyoipandisha timu hiyo.

Amesema ataongeza nyota wapya ambao wana uzoefu na Ligi Kuu ili kusaidia timu yao hiyo kutoa ushindani mkubwa katika soka la Tanzania.

“Maboresho ya kikosi yatafanyika kwa ajili ya kuongeza baadhi ya wachezaji, tutaongeza nguvu katika baadhi ya nafasi ambazo zilikuwa na upungufu, waje kusaidiana waliopo,” amesema Makata.

Amesema wamekuja kuleta ushindani, na wanafanya usajili kuimarisha kikosi chao ili kufanya vizuri katika Ligi Kuu na hawaendi kushiriki na kurudi chini kama ilivyokuwa timu zingine kucheza msimu mmoja na kushuka.

“Kikubwa ni kuendelea kupewa sapoti kutoka kwa wananchi pamoja na wadau wa soka, baada ya timu kupanda, sapoti yao ni muhimu katika kila nafasi kuanzia usajili pamoja na maandalizi ya timu kabla ya kucheza Ligi Kuu,” amesema Makata.

NEC: Uchaguzi mkuu Jumatano, octoba 28,2020
Mtibwa Sugar Vs Young Africans "Pasua Kichwa"