Tanzania inakwenda kuwa nchi ya kwanza Afrika ambayo imetekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha zake yenyewe ikiwemo mradi wa kuwasha umeme vijiji vyote nchini, kujenga reli ya kisasa, kupeleka watoto shuleni kwa takwimu kubwa pamoja na miradi mengine ambayo ni vipaumbele vinavyogusa maisha ya watu moja kwa moja.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na Dar24Media nje ya viwanja vya Bunge jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Tanzania ina miradi mingi hivyo kama nchi inafanya moja baada ya jingine kwa kuongozwa na vipaumbele.
Sambamba na hayo Nchemba ametoa rai kwa wananchi na jamii kwa ujumla kutokufanya majaribio ya kuficha uovu kwa kumaliza kirafiki au kindugu inapotokea mtoto kafanyiwa ukatili kinyume na haki za mtoto kwa kwani kufanya hivyo kunaharibu dira ya mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho kibaya.
“Hatuwezi tukaipa dhambi neno zuri au jina zuri alafu tukaitukuza”. amesema Waziri Nchemba.
Ameongeza kuwa kwa yoyote atakayefanya vitendo hivyo, (yule aliyefanya kosa na yule aliyemficha mkosaji), wote wataingia kwenye mikono ya sheria, na kusisitiza hata kwa wananchi ambaye si mtoto wako kutoa taarifa katika vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe.