Tanzania inatarajia kupata miradi ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo nishati jadidifu yenye thamani ya shilingi trilioni 42.4 kwa mujibu wa mchango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, itakayosaidia katika kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Hayo yamebainishwa leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya Kujadili Matokeo ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya siku mbili ya kujadili Matokeo ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma.
Amesema kuwa miradi hiyo itafadhiliwa na Benki ya Dunia, Taasisi ya Afrika 50 na Shirika la Nishati la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China Renewable Energies ambapo Kampuni ya Equinor iliahidi kukamilisha makubaliano ya mkataba wa ufadhili wa mradi wa gesi ifikapo Disemba 08,
2022.
Fursa hiyo imekuja kutokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwakutanisha Marais watano kutoka Zambia, Zimbabwe, Malawi, Botswana, Makamu wa Rais wa Angola na watendaji kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika katika uzinduzi wa mtandao wa uzalishaji wa pamoja wa nishati jadidifu kwa nchi za kusini mwa Afrika na kujadili fursa za uwekezaji katika sekta hiyo na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.