Serikali za Tanzania zitaendelea kuzitumia vyema rasilimali zilizopo ili ziweze kuchangia ukuaji wa uchumi na kuharakisha maendeleo ya jamii kutokana na uwepo wa mfumko wa bei nchini na Duniani kwa ujumla uliochangiwa na sababu mbalimbali.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema uchumi wa Tanzania Visiwani unategemea sekta ya utalii na kwamba hali ya vita vya Ukraine na maradhi ya Uviko 19 yalichangia athari za zilizopo.
Amesema, kutokana na tatizo hilo, Tanzania Bara na Zanzibar kwa pamoja nazo zimeathiriwa na hali hiyo na hivyo kuwepo ongezeko la bei za bidhaa mbali mbali, kupungua kwa uzalishaji na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi kutoka asilimia saba iliyokuwepo hadi kufikia asilimia 1.7.
“Hali hii pia imechangia nchi kuwa na uwezo mdogo wa kutekeleza baadhi ya miradi yake ya mendeleo sambamba na kathirika kwa bajeti kwenye utekelezaji wa masuala mbali mbali ya maendeleo,” ameongeza Rais Mwinyi kupitia hotuba hiyo.
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kuyatumia vyema majadiliano hayo kama nyenzo muhimu ya kubadilishana uzoefu na maarifa katika kuweka mipango na mikakati imara ya pamoja kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekata mbali mbali za maendeleo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa mkutano huo utasaidia kuongeza uelewa kwa wadau na washirika mbali mbali wa maendeleo juu ya mafanikio na changamoto mbali mbali zilizopo na kufikiria njia bora za kuzitatua.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum, amesema mkutano huo ni muhimu katika kutathimini jitihada za kiuchuimi na changamoto zilizopo ikiwemo kuongeza kasi kwa kushirikiana na Wadau mbali mbali wa maendeleo ili kufanikisha malengo na mipango ya nchi.
Mkutano huo wa Siku mbili, ambao umeandaliwa na Wizara za Fedha za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo washirika wa maendeleo, mabalozi , watafiti, wachumi, wasomi wa Vyuo Vikuu na wanadiaspora.