Baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati (CECAFA) hii leo limethibitisha kufanyika kwa michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati (Kombe La Kagame) mwaka 2018.

Michuano hiyo iliyokua kimya kwa miaka miwili, imetangazwa kufanyika jijini Dar es salaam, Tanzania kuanzia Juni 28 hadi Julai 13.

Katibu mkuu wa CEFACA Nicolas Musonye amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa, michuano hiyo itafanyika kwenye viwanja vya Taifa na Azam Complex, Chamazi.

Musonye amesema wamelazimika kufanya michuano hiyo sambamba na Fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, kwa sababu wasipofanya mwezi huu hayatafanyika tena kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Musonye ameishukuru Tanzania kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa kusema kuwa, anatarajia michuano hiyo itafana kwa sababu ya rekodi ya nchi hiyo kuandaa mashindano yaliyokuwa na msisimko mkubwa miaka ya nyuma.

Pia amewapongeza Rwanda na Rais wao, Paul Kagame kwa kuwa wadhamini wa mashindano haya kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu huyo wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye amesema kutakua na makundi matatu.

Kundi la kwanza linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC wa Sudan Kusini. Wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti na Kundi lina timu za Simba, Young Africans Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.

Mbunge wa CCM awafananisha wapinzani na Mbwa
Mwalimu amdhalilisha kingono mwanafunzi shule ya msingi