Tanzania, inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa pili wa kutokomeza ukeketaji ambao utakao hudhuriwa na washiriki 900 kutoka Mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika utakaofanyika kuanzia Oktoba 9 – 11, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema wakati wa mkutano huo, pia kutakuwa na Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ambayo hufanyika Oktoba kila mwaka.

Amesema, “Tanzania tumepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa kutokomeza Ukeketaji ambapo kama nchi tutakuwa na washiriki 200 kutoka mikoa yetu yote na Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika na Mabara mengine watakuja washiriki 700.”

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima amefafanua kuwa Mkutano huo utakaokuwa na Kaulimbiu isemayo “Mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji,” utatoa fursa kwa wadau wanaopambana na ukeketaji kuunganisha nguvu za pamoja, kubadilishana uzoefu, kujengeana uelewa na maarifa katika kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji kwa nchi za Afrika.

Maadhimisho hayo ni ya 12 sasa, na ni utekelezaji wa Tamko la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 66/170 la Desemba 19, 2012 ambapo lengo la siku hiyo ni kutathmini jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuboresha upatikanaji wa Haki, Ulinzi, Ustawi na Maendeleo ya Mtoto wa Kike.

Wafanyabiashara washauriwa kufunga Kamera za ulinzi
Tuzo: Malawi yaukubali mchango wa Tanzania