Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe.  Mwanaidi Ali Khamis amekemea vikali vitendo vya ukeketeji kwa watoto kike na kuwataka wanaojihusisha na ukatili huo kuacha mara moja. 

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akihitimisha hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukeketaji nchini na kuwataka Wadau wote kuendelea kupambana katika kutokomeza ukeketaji na kuongeza kuwa, Serikali inatambua Mchango wao katika kuwakomboa Mabinti waishio katika mila hizo zilizopitwa na wakati.

 “Ukeketaji si jambo zuri na linawakosesha mabinti fursa kwani wanashindwa kujiamini kabisa,vitendo hivyo ni dhambi na havipo kwenye vitabu vya dini na pia ni uonevu wa hali ya juu  hivyo Jamii iachane na vitendo hivo,”Amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Awali akizingumza katika uzinduzi wa Mkakati huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema Mila na Desturi za kuwaanda watoto wa kike kuelekea utu uzima zinaweza kufanyika kwenye Jamii bila kufanya Ukeketaji.

“Kuna mambo ambayo ni mazuri ya kuwaanda vijana lakini kitendo kisichofaa ni ukeketaji, tunayo kazi kubwa ya kufanya ambayo ni kubadili fikra za jamii na ikiwezekana kutafuta namna mbadala ya kuendeleza Mila na Desturi zetu,” Amesema Katibu Mkuu Jingu.

Akiwasilisha Mpango kazi wa kutekeleza Mkakati huo kwa Wadau walioshiriki uzinduzi, Meneja Mradi wa kutoa elimu kuhusu Ukeketaji na afya ya uzazi wa Shirika la AMREF HEALTH AFRICA, Dkt. Jane Semfano  amesema vitendo vya Ukeketaji nchini vimepungua huku akionesha takwimu za 1996 ilikuwa ni asilimia 18 na utafiti wa mwaka 2015/16 ulionesha kwamba msichana mmoja kati ya 10 ndiyo amekeketwa. 

Mmoja wa Mangariba aliyestaafu kazi hiyo kutoka Mkoa wa Singida Hawa Hussein amesema kitendo hicho ni hatari kubwa kwa sababu ameshuhudia madhara mengi ikiwemo vifo kupitia mikononi mwake hivyo amewaasa Mangariba wote kuacha vitendo hivyo.

PICHA: Kocha Franco atinga kambini
Mitaala ya Elimu kupitiwa upya