Tanzania na Afrika Kusini zimedhamiria kukuza ushirikiano katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa Ushirikiano uliosainiwa mwaka 2011.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja na wajumbe wa kamati ya Maandalizi kutoka Tanzania na Afrika Kusini, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Haji Janabi amesema kikao hicho ni hatua za awali katika kufikia azma hiyo ya kufanyika kwa Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini hapa nchini.
“Dhima kuu ya tamasha hilo ni kuwa na jukwaa la kuonesha vipaji vya Sanaa na Utamaduni, kukuza ushirikiaano wa kikanda, kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini, maonesho ya mavazi, mihadhara ya umma pamoja na midahalo yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii baina ya nchi hizi mbili,” amesema Janabi.
Awali, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa kutoka Idara ya Michezo Sanaa na Utamaduni Afrika Kusini, Ruphus Matibe amesema msimu huo wa Utamaduni wa Afrika Kusini nchini Tanzania unataraiwa kuanza na tamasha hilo ambalo litafanyika Novemba 17 hadi Desemba 04, 2022.
Amesema, “Tamasha hili linalenga kuwakumbusha watu wa nchi hizo mbili historia yao njema tangu enzi za Harakati za Ukombozi chini ya Waasisi wa mataifa hayo mawili chini ya waasisi Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.”
Aidha, amefafanua kuwa, “Tupo hapa kuunganisha watu wa Afrika Kusini na wazee wao, Tanzania hatukupewa tu ardhi wakati wa harakati za Ukombozi, tulipewa mahali pa kuishi kulingana na ukarimu wa watanzania wakiongozwa na Hayati Mwl. Julius Nyerere.”
Ameongeza kuwa wazee wa mataifa hayo waasisi na wananchi wa mataifa hayo wakati huo walitekeleza wajibu wao wa kuhakikisha wamejenga umoja katika nchi zao hatua iliyosaidia kupatikana uhuru na kusisitiza kuwa Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini nchini Tanzania ni moja ya fursa kwa kizazi cha sasa kutatua changamoto za kiuchumi zinazokabili nchi za Afrika.
Kuhusu kukienzi Kiswahili ambayo ni lugha ya kazi sasa katika Umoja wa Afrika (AU), Matibe amesema Afrika Kusini wapo mstari wa mbele kufundisha lugha ya Kiswahili kwa shule za msingi nchini humo.
Tayari nchi hizo mbili zimesaini mkataba wa makubaliano ya kufundisha somo hilo Julai 07, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.
Afrika Kusini nchini Tanzania kutoka Tanzania na Afrika Kusini wakiwa katika picha ya
pamoja mara baada ya kikao cha maandalizi ya Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa
Afrika Kusini nchini Tanzania.
Utekelezaji wa Mkataba huo baina ya nchi hizo mbili unakuja na utaratibu wa kuwa na Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini nchini Tanzania ambalo lengo lake ni kuunga mkono juhudi za kupanua wigo wa utalii, biashara za bidhaa na huduma za kiutamaduni.
Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini linatarajiwa kufanyika katika maeneo manne nchini yaliyobeba Historia ya Afrika Kusini katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Zanzibar.