Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amefungua Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Msumbiji unaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 22 -24 Agosti, 2022.
Mkutano huo, ulioanza Agosti 22, 2022 katika ngazi ya Wataalamu utafuatiwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu, na baadaye mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika Agosti 24, 2022 Jijini Dar es salaam.
Akifungua mkutano huo, Balozi Sokoine amewaomba watendaji kutoka Tanzania na Msumbiji kutumia mikutano ya JPC, kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuweka mazingira wezeshi ili sekta za umma na binafsi ziweze kuwekeza kwenye uchumi wa kila nchi kwa maendeleo endelevu na kuinua uchumi wa nchi zote mbili.
Aidha, Balozi Sokoine pia ametumia mkutano huo kuihakikishia Msumbiji juu ya imani iliyonayo Tanzania katika uhusiano wao, na kwamba itaendelea kuulinda na kuimarisha uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Tanzania ina imani na uhusiano iliyonao na Msumbiji na itaendelea kuulinda uhusiano huo na ni dhamira yetu kuwa tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu ambao ni wa kindugu na kihistoria kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisisitiza.
Hata hivyo, ametoa shukurani kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi kwa jitihada zao za kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Tanzania na Msumbiji, zinashirikiana katika sekta za Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha, Nishati, Maendeleo ya Jamii, Afya, Kazi, Ujenzi wa Miundombinu, Uchukuzi, Sayansi, Teknolojia, Habari, Elimu,Utamaduni na Sanaa, Biashara na Uwekezaji, Utalii na Wanyamapori, Kilimo, Uvuvi, Maji, Mazingira, Madini, Afya, Mifugo, Nishati na Elimu.
Tume hiyo ya Kudumu ya Pamoja (JPC), kati ya Tanzania na Msumbiji ilianzishwa mwaka 1979 na tangu wakati huo jumla ya mikutano 14 imefanyika ambapo maeneo ya ushirikiano yalikuwa yanajadiliwa na kukubaliwa kwa pamoja. Maeneo hayo ni Uhusiano wa Kidiplomasia, Biashara, Mawasiliano, Uchukuzi, Uhamiaji, Ulinzi na Usalama, Kilimo, Utalii na Uvuvi.