Kocha Mkuu wa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ Mohamed Abdallah ‘Baresi’amesema wapo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC, ikiwa ni sehemu ya harakati zao za kutaka kujinusuru kushuka Daraja mwishoni mwa msimu huu.
Tanzania Prisons inashika nafasi za mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na imekuwa katika hekaheka za kujinasua kwenye nafasi hizo, ili isalie katika Mshike Mshike wa Ligi hiyo msimu ujao wa 2023/24.
Kocha Bares amesema baada ya kupoteza mchezo wa hatu ya 16 Bora Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya mabingwa watetezi Young Africans iliyoshinda 4-1, amekiandaa vizuri kikosi chake huku akimaliza tatizo la safu ya ushambuliaji kushindwa kutumia vizuri nafasi wanazopata.
Amesema kutopata ushindi katika michezo minne aliyosimamia alikuwa akitafuta muunganiko na kuwaandaa kisaikolojia vijana wake, lakini pia kuondoa makosa ya kuruhusu mabao mengi kwenye michezo inayowakabili.
“Kwa sasa naona nimefanikiwa kutengeneza nafasi kilichobaki ni namna ya kuzitumia. Ninaamini kuanzia mchezo wa Jumamosi dhidi ya Namungo tunaanza kuhesabu pointi tatu hadi mchezo wa mwisho msimu huu,” amesema Baresi.
Wajelajela hao hawajawa na matokeo mazuri wakicheza michezo 24 na kuwa nafasi ya 14 kwa kufikisha alama 22, ambapo Jumamosi hii watakuwa ugenini kuwakabili Namungo FC ambao wapo nafasi ya saba na alama 32.