Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kukabidhi rasmi kijiti cha uenyekiti wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC kwa Rais wa Msumbiji Philip Nyusi Agosti17, 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 15, 2020 Dkt. Hassan Abbasi ambaye ni msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania amesema baada ya mwaka mmoja wa mafanikio na kazi kubwa ya kuongoza jumuiya muhimu katika ukanda wa afrika SADC, Rais Magufuli atakabidhi kijiti kwa mafanikio makubwa kwa Rais Philip Nyusi.
Amesema, katika makabidhiano hayo, Rais Magufuli ataeleza kwa kina mafanikio ya Tanzania katika kuiongoza jumuiya hiyo.
“Rais Magufuli yeye mwenyewe ataeleza mafanikiko kwa kina ya ajenda gani tulisukuma na maamuzi gani yamefanyika katika jumuiya ya SADC na yamekuwa na manufaa gani kwa wananchi wa nchi 15 za jumuiya hiyo”. Amesema Dkt. Abbasi.
Makabidhiano ya uenyekiti wa SADC kwa nchi ya Msumbiji yalianza wiki iliyopita, ambapo alhamisi tarehe 13 Agosti 2020, Prof Paramagamba Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje ya Tanzania alikabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji ambaye aliwakilishwa na Balozi wa Taifa hilo Nchini Tanzania Monica Clemente.