Tanzania imetajwa kuwa moja kati ya nchi 10 za Afrika zitakazonufaika na kiasi cha Euro bilioni 44 za Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Umoja wa Ulaya (EU) na Ushirikiano wa Ufalme wa Hispania umeahidi kutoa fedha hizo kupitia Mkakati Mpya wa Tatu Afrika (Third African Plan), ambao utajikita katika kusaidia miradi kwenye sekta ya maji, afya, utalii na michezo.
Mkurugenzi Mkuu wa Afrika katika Wizara ya mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya na Ushirikiano wa Ufalme Hispania, Raimundo Rubio, jana aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa lengo la mkakati huo ni kusaidia maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi barani Afrika.
“Kwa Tanzania miradi itakayotekelezwa ni pamoja na mradi wa maji katika Halmashauri ya Mbozi, vijiji 12 kutoka kata ya Malangali Iringa na vituo mbalimbali vya Afya” Alisema, Rubio.
Aliongeza kuwa Umoja wa Ulaya umelenga kutumia ‘Mkakati wa Tatu Afrika’ ili kuimarisha ushirikiano katika nchi hizo na ziapata fursa ya kunufaika na miradi hiyo pamoja na uwekezaji kwa pamoja.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi alisema hivi karibuni nchi ya Hispania imeona Tanzania ni moja kati ya nchi za Afrika zenye fursa.
“Umoja wa Ulaya umeweka mkazo katika miradi ya maji, ujenzi wa vuto vya afya na hospitali na pia kuwekeza katika sekta ya utalii…Hispania ni moja ya nchi iliyopiga hatua kubwa sana katika sekta ya utalii barani Ulaya,” alisema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi aliongeza kuwa Tanzania itashirikiana na Hispiania kuwekeza katika viwanda vya dawa ambapo kwa namna moja au nyingine nchi yetu itaendelea kuimarisha sekta hii muhimu. “Maeneo mengine ni sekta ya Michezo ambapo tunaamini pia kuimarisha sekta ya michezo, na kupata watawala wa michezo na waongozaji wa michezo hapa nchini watakuza kiwango cha mpira zaidi,” Alisema Prof. Kabudi
Kwa mujibu wa Bw. Rubio, nchi kumi za Afrika ambazo zinategemea kunufaika na fursa hiyo ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria, Ethiopia, Senegal, Ghana, Ivory Coast, Tanzania, Kenya, Angola and Msumbiji.