Tanzania imelaani vikali vikwazo ilivyowekewa nchi ya Zimbabwe na kuitaka dunia kuiondolea nchi hiyo vikwazo bila masharti kwani haviiathiri Zimbabwe peke yake bali huathiri nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kauli ya kulaani vikwazo hivyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika kongamano maalum kuhusu ‘vikwazo vya kiuchumi na hatma ya Afrika: Uzoefu wa Zimbabwe,’ leo Jijini Dar es Salaam.
“Tulikubaliana katika mkutano wetu wa mwezi Augosti kuwa leo tarehe 25/10/2019 kuiambia dunia kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi ilivyoviwekea bila masharti..…leo siyo siku ya kuomba wala kukumbushana bali leo ni siku ya kuiambia dunia rasmi iiondolea Zimbabwe vikwazo vya kuichumi,” Amesema Prof. Kabudi
Aidha alisema kuwa wapo wanaosahau sababu ya msingi iliyoifikisha Zimbabwe katika maamuzi iliyoyachukua ambayo kiini chake kikubwa ni suala la ardhi.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, mzizi wa mambo yote haya ni sheria ya kibaguzi iliyopitishwa na waingereza kwa kusingizia kuwa wameipa Zimbabwe utawala wa ndani mwaka 1923 lakini wao walibaki na mamlaka yote juu ya ardhi. Amesema sheria ile ilikuwa ya kibaguzi kwani ilichukua zaidi ya nusu ya ardhi yote ya Zimbabwe.
“Ni wajibu wetu sisi kama Tanzania kuendelea kusimama na Zimbabwe, ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa Zimbabwe inaondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa” amesema.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia na Wazee, Prof. Jingu alisema kuwa diplomasia ya uchumi imeiwezesha Tanzania kuingia katika uwekezaji, kusaini mkataba, msaada au masoko hivyo tunapaswa kuhakikisha kuwa masuala ya kiuchumi yanapewa uzito wa hali ya juu.
“Vita ya kiuchumi imekuwa na athari mbalimbali kwa wananchi kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa ujumla….vita hii ya Zimbabwe kuwekewa vita ya kiuchumi imeleta athari nyingi baadhi ni kukusekana kwa maji safi na salama, kukosekana kwa nishati ya uhakika na ongezeko la mfumuko wa bei ambao umeathiri si tu Zimbabwe, bali hata nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe vimesababisha anguko kubwa na adha kwa wanachi masikini tena wasio na hatia.