Serikali imeridhia ombi la Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Prof. Remy Ngoy Lumbu la kuitaka Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 77 utakaojumuisha nchi wanachama wa kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na watu utakaofanyika Oktoba, 2023.
Prof. Lumbu alitoa ombi hilo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wakiongelea mambo mbalimbali kuhusiana na masuala ya Haki za Binadamu na Watu.
Aidha, Prof. Lumbu alipongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza ambapo makundi mbalimbali yameonekana kupewa nafasi ya kujieleza yakiwemo ya wanasiasa na suala la uhuru wa vyombo vya Habari.
Awali, Rais Samia alimueleza Prof. Lumbu kuwa anaamini matatizo ya Afrika yanaweza kumalizwa na waafrika wenyewe na kwamba alikutana na vyama vya upinzani kuangalia uwezekano wa nini kifanyike na kuwa na kauli moja.