Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani (UNDP), nchini Tanzania limetekeleza kwa vitendo wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka vijana kupatiwa stadi za msingi nje ya darasa kama njia mojawapo ya kuwawezesha kumudu maisha yao ya baadaye.
Mkuu wa Chuo Chuo cha Ufundi stadi Kibosho, Daniel Mboya amesema miongoni mwa stadi ni kilimo cha majani ya kulisha mifugo, zinatolewa kwa vijana ili watambue namna wanavyoweza kutumia maji na virutubisho vingine vyote isipokuwa udongo.
Mboya amesema “Kilimo hiki, kinatusaidia sisi kwenye shughuli za kilimo kwani ufugaji tunaofanya hapa shuleni tumepunguza gharama za ufugaji kwani hayo majani yanalisha mifugo yetu, na mifugo inatupatia mazao mengine kama vile mbolea na maziwa.”
UNDP, imekisaidia chuo hicho kwenye kilimo cha mboga na matunda kupitia Chama cha wakulima wa mboga na matunda Tanzania (TAHA), ambapo Wanafunzi wamekuwa wakipeleka ujuzi kwa wazazi na jamii.
“Wanafunzi wetu wengi wanatoka tarafa ya Kibosho, kwa hiyo nao wanatumika kwenda kutoa mafunzo pia kwa wazazi wao na vikundi vilivyoko huko kwao,” amefafanua Mkuu wa chuo hicho Mboya.
Amesema stadi wanazofundishwa vijana zinalenga kuwawezesha kujitegemea baada ya mafunzo, na kwamba taaluma hiyo imewasaidia wengi kuondokana na utegemezi kwa kujibidiisha kufanyia kazi kile walichojifunza ambacho kimewaletea manufaa maishani.
Mradi huo wa UNDP, pia unawapatia vijana stadi za kuongezea thamani mazao ambapo wanafunzi na wanajamii wamependa ufanisi wake kutokana na kufundishwa namna ya kukausha na kufungasha mazao.
“Mfano kutengeneza unga, na pia kuna siku za wakulima wanakuja kutembelea mashamba au miradi yetu na kujifunza na wameleta thamani kwenye maisha ya wanafunzi na jamii yetu” amefafanua Mboya.
Kwa mujibu wa UNDP, matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo kama vile umwagiliaji na mashine za kuvunia, huongeza thamani kwenye mavuno na hatimaye wakulima kuuza mazao yao na kujipatia kipato.