Serikali imepanga kupeleka umeme katika migodi 336 nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa gharama ya shilingi Bilioni sita ili kazi za uchimbaji wa madini nchini zifanyike kwa tija na kukuza uchumi wa nchi.

Waziri wa Nishati, January Makamba ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita wakati akikagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Wizara, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema, TANESCO ina mkakati wa kufikia migodi mingi kupitia mradi wa gridi mapato ulio na na shilingi 300 bilioni, ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na viwanda.

Waziri Makamba pia amekagua kazi ya upelekaji wa umeme katika mgodi wa dhahabu wa Geita na kueleza kuwa utaanza kutumia umeme wa gridi kuanzia machi 2023.

“Mgodi huu unahitaji megawati 40 na tangu umeanza kufanya kazi umekuwa ukitumia jenereta za dizeli kuendesha mitambo, hivyo TANESCO italeta umeme wa gridi kutokea kituo cha mjini Geita pamoja na cha Mpomvu na TANESCO itapata mapato,” amebainisha Waziri Makamba.

Akiwa katika kijiji cha Shilungule kwenye Jimbo la Busanda, Waziri wa Nishati alitembelea zahanati ya kijiji hicho yenye changamoto ya utoaji huduma kutokana na kukosa umeme na kuwaagiza REA kufunga mitambo ya umeme jua wakati zahanati hiyo inasubiri kusambaziwa.

Waziri Makamba pia amefanya ziara katika Wilaya ya Chato na kuzungumza na wananchi wa eneo la Buselesele ambapo aliahidi kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vilivyosalia wilayani humo pamoja na kuweka taa za barabarani.

Ziara ya Waziri wa Nishati mkoani Geita pia ilihusisha ugawaji wa mitungi ya gesi kwa vikundi mbalimbali vya wanawake katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Busanda na Chato ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

DC akemea watoto kufanya biashara, ataka waende shule
Tanzania yatekeleza kwa vitendo stadi za kazi nje ya darasa