Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema usimamizi makini wa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imewezesha Taifa kuvuka malengo ya kupambana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI – VVU, ya 95-95-95 yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2025.
Majaliwa ameyasema hayo alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa Juu ya Kuimarisha Ubia Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa Uendelevu wa Mafanikio ya Mwitikio wa UKIMWI nchini, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
Amesema, “tayari asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi ya VVU wanajua hali zao, asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya ARV na kati yao, asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye damu. Jukumu tulilonalo ni kulinda na kuyaendeleza mafanikio haya hadi tufikie malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030.”
Aidha, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za UKIMWI ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) na mipango mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla ili malengo ya kutokomeza ugonjwa huo yaweze kufikiwa.
Kuhusu majumuisho yaliyotokana na mdahalo huo, Waziri Mkuu amewahakikishia wadau na Watanzania wote kuwa Serikali imesikia na kupokea yote yaliyotajwa katika mdahalo huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) na itayafanyia kazi.