Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Sekta ya Viwanda ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya Watanzania
Aidha Makamu wa Rais Dkt Mpango amehimiza kuhakikisha soko la uhakikia la malighafi linapatika nchini lakini hata kutoa Ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya serikali pamoja na fedha za kigeni.
Dkt. Mpango amesema hayo Oktoba 08, 2021 katika hafla ya kutoa Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa Viwanda nchini (Presidental Manufacturer of the Year Award – PMAYA) zilizoandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara iliyofanyika katika ukumbi wa Serena Hoteli Dar es salaam.
“Sekta ya viwanda ndio chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali na ni mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuongeza thamani ya malighafi tulizonazo, kutoa ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni na kuongeza na kuboresha sayansi na teknolojia,” Amesema Makamu wa Rais Dkt Mpango.
Aidha amesisitiza kuwa Sekta ya viwanda ina jukumu la kuhakikisha tunapenya Zaidi katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na lile la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuhakikisha uuzaji wa bidhaa katika soko la EAC unaongezeka kufika asilimia 15 ukilinganisha na asilimia 07 ya sasa na kwa upande wa SADC lengo ni kuhakikisha tunauza asilimia 30 ya soko lote ukilinganisha na asilimia 14 ya sasa.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dkt Mpango ametoa rai kwa wananchi wote kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kwa upande Wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ametumia nafasi hiyo kutoa kanzi data ya viwanda nchini ambapo ameeleza kuwa kufika Julai 2021 kuna viwanda 80,969 ambavyo viwanda vidogo sana ni 62,400, viwanda vidogo 17,267, viwanda vya kati ni 684 na viwanda vikubwa 618.
Vilevile, Prof. Mkumbo ametoa taarifa ya Maendeleo ya Sekta ya Viwanda nchini kwa kubainisha kuwa ripoti ya benki kuu ya taarifa za kiuchumi za kila mwezi inaonesha kwamba kufikia Julai 2021 Tanzania imeuza nje bidhaa za viwandani zenye jumla ya Dolla za Kimarekani Bilioni 1.12 ambayo ni kwa mara ya kwanza kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 4.