Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Ubalozi na Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa jijini Vienna nchini Austria.
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo ni mafanikio yanayoimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo jijini Vienna na kinaonesha jinsi Tanzania inavyoipa kipaumbele Austria.
“Kufunguliwa kwa Ubalozi huu ni mafanikio makubwa ambayo yanaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo hapa jijini Vienna na kinaonesha kwa vitendo kuwa Tanzania inaipa kipaumbele Uhusiano wake na Austria,” alisema Dkt. Tax.
Ameishukuru Serikali ya Austria na Wizara inayoshughulikia masuala ya Ulaya na uhusiano wa Kimataifa kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi wa Tanzania Vienna tangu ulipoanzishwa hadi kufikia siku ya uzinduzi.
Amesema Serikali ya Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao wanapambania agenda moja za kulinda na kukuza amani na usalama pamoja na kupambana na uhalifu wa kupangwa, rushwa, ugaidi na amewaomba kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya watu wote.
“Serikali ya Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao tunapigania agenda moja, ajenda hizi ni kama kulinda na kukuza amani na usalama, kupambana na uhalifu wa kupangwa, rushwa, ugaidi na mengine mengi , nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya watu wote,” alisisitiza Dkt. Tax.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo jijini Vienna Naibu Waziri anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa wa Austria, Peter Launsky-Tieffenthal amesema Austria inapongeza uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kufungua Ubalozi wake Austria na kuungana na nchi nyingine 16 za Afrika zenye Ubalozi nchini humo na kuahidi kuusaidia Ubalozi huo kwa kila hali ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.