Mchezaji wa Zamani wa timu ya Simba SC na timu ya Taifa ya Tanzania, Arthur Mambeta amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa saratani kwa kipindi kirefu na kumsababishia kukatwa miguu yote miwili.

Afisa habari wa Simba Haji Manara amesema wamepokea ujumbe huo kwa mshtuko mkubwa kifo cha mchezaji huyo ambapo msiba wake utafanyikia Kigamboni.

Tumepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha mchezaji wa zamani wa kimataifa wa klabu yetu ya Simba Arthur Mambeta ambae amefariki jana hapa jijini. Mambeta anakumbukwa sana na wanasimba pale alipotoka kwenye kustaafu soka na kuja kuisaidia klabu yake kuifunga klabu ya Yanga kwenye mchezo wa fainali Ligi kuu goli 1-0. Hiyo ilikuwa mwaka 1973 huko nyuma mchezaji huyo alikuwa ni mshambuliaji mahiri kabla ya kuja kucheza beki, amesema Manara.

 

Mambeta alianza kuchezea Simba SC miaka ya 1960 enzi za Sunderland na wakati wake alikuwa kiungo mshambuliaji hodari kuanzia klabu yake hadi timu ya taifa.

Na Arthur Mambeta ndiye mchezaji pekee wa Tanzania aliyekuwemo kwenye kikosi cha kwanza cha kombaini ya Afrika Mashariki iliyocheza na West Bromwich Albion ya England mwaka 1974 Uwanja wa Nakivubo mjini Kampala, Uganda.

Mambeta alindelea kujihusisha na mchezo katika utawala na amewahi kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi Simba SC.

Hata hivyo, Mambeta alianza kujitoa taratibu kwenye soka baada ya kuanza kusumbuliwa na maradhi ya saratani yaliyosababisha akatwe miguu yake yote miwili.

Uongozi wa Dar24, unatoa pole kwa familia na ndugu, jamaa na marafiki kwa kumpoteza mtu muhimu, Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi.

TCRA: Usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kuanza rasmi
Tanzania yakata ushirikiano na Korea Kaskazini