Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amekutana na wadau wa Sanaa mbalimbali nchini katika kujadili maendeleo ya tasnia hiyo zikiwepo haki za wasanii na jinsi ya kuboresha tasnia ya Sanaa na muziki ili wasanii waweze kufaidika kwa kile wanachokifanya.
Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri Mwakyembe amesema kuwa Serikali ipo tayari kupokea mapendekezo ya wasanii kuhusu kuunganisha nguvu katika vyombo vya wasanii ambavyo ni COSOTA, Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania ili waweze kuhudumia wasanii kwa maendeleo ya kazi zao.
“Sisi tunawaletea mawazo tu, si Sheria, si Mswada ni mawazo ambayo yatamilikiwa na ninyi baada ya kuyapitisha, na ninyi kama wadau wa Sanaa na muziki waliohudhuria kwenye mkutano huu mnatakiwa kutoa mawazo yenu ili Tasnia hii iweze kufikia katika muafaka mzuri ambao utaboresha kazi za wasanii na kutetea maslahi ya kazi zao,” amesema Dkt. Mwakyembe.
Amesema kuwa Tasnia ya Sanaa na Muziki imekuwepo muda mrefu na imekuwa kimbilio kwa vijana wengi, lakini imekuwa ikitajirisha baadhi ya watu na wengine kuachwa nyuma kimaendeleo, kwa hiyo mabadiliko katika Tasnia hiyo hayana budi kutokea ili kuleta ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa mabadiliko hayo hayalengi kuvunja au kuingilia Mamlaka ya vyombo hivyo, bali lengo lake ni kusogeza huduma karibu kwa ajili ya kurahisisha kazi kwa wasanii na wadau wote wa Sanaa Nchini.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa mabadiliko hayo yatafanya vyombo hivyo kuwa na lugha moja ili kuepuka wasanii kukamatwa au kufungiwa pale wanapokuwa wanafanya kazi zao kutokana na utofauti wa kanuni na Sheria zilizopo.
“Kipindi cha mabadiliko kimefika, Watanzania tusiogope kufikiri katika tasnia hii, kwa muda mrefu imekuwa ikisaidia sana lakini haiwezi kuwafaidisha wachache na wengine wabaki masikini, haiwezekani ni lazima tufikirie njia itakayo tusaidia wote,” amesema Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho Tanzania, William Frank Chitanda, amesema kuwa Mabadiliko ya kuiunganisha Basata na Bodi ya Filamu ziungane na COSOTA ihamishiwe Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara yatasaidia pakubwa tasnia hiyo.