Shirika la Viwango Tanzania TBS limetoa wito kwa Taasisi binafsi na za kiserikali zinazojihusisha na ugezi, ithibati ya ubora kwenda kupata mafunzo ya ithibati ili kuwawezesha kuweka mifumo ya kimataifa katika utendaji wa kazi zao, utakaosaidia kuepuka vikwazo vya kimataifa kwenye biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu anaesimamia dawati la ithibati Stella Mroso, amesema kuwa ithibati inaweza kutolewa kwenye taasisi za upimaji, ukaguzi, uthibiti wa ubora ikiwa na lengo la kujenga imani kwa watumiaji wa bidhaa au huduma kuona inafaa kwa matumizi, huku akiieleza kuwa ithibati ni nyenzo muhimu katika kuondoa vikwazo vya kibiashara kitu ambacho kitachangia kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha Stella ameelezea manufaa ya kutekeleza mifumo ya kiwango cha kimataifa katika maabara za upimaji za ugezi ambapo moja ya manufaa ni kujenga imani kwa wateja, kuziwezesha maabara kufafanua na kuainisha kazi zao lakini pia kuweka malengo ya ubora katika kufikia malengo ya taasisi.
Hata hivyo ameelezea ni maandalizi gani kama maabara wanatakiwa kuwa nayo ambapo kabla ya kuomba cheti cha ithibati ya umahili moja ya maandalizi ni kupata uelewa wa matakwa ya viwango husika kwa kupatiwa mafunzo ambayo yanatolewa na TBS, hatua nyingine ni kufuata matakwa ya yaliyowekwa ya kimataifa.