Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA, Hamza Johari amesema ndege aina ya Embraer 190 5H-FJH iliyozuiwa nchini Tanzania na waliokuwa wafanyakazi wake haiwezi kutumika kulipa madeni wanayoidai kampuni hiyo.
Hamza amesema kuwa ndege hiyo haitalipa madeni kwa kuwa haikuwa mali ya shirika hilo, ingawa katika ombi lao wafanyakazi hao, katika vyombo vya sheria walipewa zuio la ndege hiyo mpaka madeni yao yalipwe.
Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo baada ya waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kujitokeza hadharani na katika mahojiano maalumu na Dar 24 wakisema wanaidai ndege hiyo zaidi ya sh bilioni 5, na sasa ndege hiyo waliyokuwa wameiweka kama dhamana imefutiwa usajili na kuruhusiwa kuondoka nchini.
“Kilichotushtua sasa ni kuwa ndege hiyo tuliyoizuia wakati tunashughulikia kesi hizo imefutiwa usajili Tanzania maana yake inaweza kuondoka Tanzania mda wowote, na hatukua tumekaa, tulikua tunahangaika, tunatafuta ushauri maana yake haki yetu inapotea”, alisema Mamy.
Aidha mkurugenzi huyo amesema kuwa ndege hiyo bado inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, na bado ipo nchini lakini sio kwa ajili ya kulipa wafanyakazi.
“Ndege hii sio mali ya Fastjet, haiwezi kutumika kulipa madeni ya wafanyakazi, Fastjet waliikodi na mwenyewe akiitaka itaondoka, wao wafanyakazi wanatakiwa waendelee kufuatilia kwa Mufisili ili mali nyingine za kampuni hiyo zitakapouzwa ndio walipwe,” alisema Hamza.
Akiongezea katika maelezo hayo, Hamza pia alisema ndege hiyo haijabadilishiwa usajili ila ilibadilishiwa vibandiko kwa muda na sasa vimerudishwa kama awali, na bado ipo nchini Tanzania.
Nae Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Paschal Katambi, alipokutana na wafanyakazi hao, baada ya kuwaahidi alipozungumza nao kwa njia ya simu, amewaahidi kulifutilia kwa ukaribu suala lao na kuwaasa wafanyakazi wote wawe na tabia ya kusema mapema wanapoanza kuona dalili za kukopwa misharahara.
“Wafanyakazi wote nawaasa muwe mnapiga kelele mapema, unapoanza kuona unakopwa mshahara kwa miezi miwili tu anza kupiga kelele, fuata taratibu za kisheria za kazi ili serikali iingilie mapema na kusaidia kabla kampuni husika haijaanza kuweka malimbikizo,” alisema Katambi.
Takribani wafanyakazi 105 waliokuwa kwenye kampuni ya FastJet wanadai maslahi yao ambayo hawakuwa wamepewa wakati kampuni hiyo ikiacha kufanya kazi hapa nchini Tanzania tangu mwaka 2018 mwishoni na mara ya mwisho kulipwa stahiki zao ilikua Januari 2019.