Vinara wa Muungano wa Kenya Kwanza nchini Kenya wamekubali kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kama mpeperushaji wao wa bendera ya urais katika Uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti 2022.

Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula akizungumza Jumamosi, Machi 19, mtaani Dundori eneo la Bahati, kaunti ya Nakuru, amesema DP Ruto atashindana na kinara wa ODM Raila Odinga kuwania kiti cha juu.

Wetang’ula ambaye pia ni Seneta wa Bungoma na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi walikuwa wametangaza nia za kugombea urais na sasa ni wazi kuwa wawili hao wamezima ndoto zao ili kumuunga mkono Ruto.

Mrengo huo sasa una kazi ya kumchagua mgombea mwenza wa Ruto jambo ambalo ni mjadala katika muungano huo huku viongozi wa vyama vinavyoegemea Kenya Kwanza Wakikataa kuvunja vyama vyao na kujiunga na chama cha UDA.

Wakati hayo yakiendelea, Naibu Rais William Ruto kwa mara nyingine amemkashifu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumtenga na kumpendelea kinara wa ODM Raila Odinga.

Ruto alisema hatua ya Uhuru kumuunga mkono Raila ndio usaliti mkubwa zaidi ikizingatiwa changamoto zile walizopitia pamoja na rais.

Hata hivyo, akizungumza katika mkutano wa siasa wa Kenya Kwanza, Murang’a, Naibu Rais alisema hatasaliti urafiki ambao ameukuza na Uhuru kwa zaidi ya miaka ishirini.

“Tumepitia changamoto nyingi pamoja ikiwa ni pamoja na kukabili kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko Hague. Tulikabiliana na Raila pamoja 2013 na 2017. Ilikuwa makosa kunitenga na Raila,” Ruto alisema.

Katika hotuba yake ya Jumapili, Machi 20, Ruto alimhakikishia rais kwamba atalinda urithi wake na wa familia yake iwapo atachaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Agosti 9.

Utafiti uliofanywa kati ya Machi 9-12 unaonyesha kuwa Azimio uliungwa mkono na asilimia 51 chama cha ODM kinachoongozwa na Raila ndicho chama kinachopendelewa zaidi ya waliohojiwa huku Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto uliibuka wa pili na asilimia 23.

Faru Rajabu aaga dunia
TCAA:Ndege Fastjet haitalipa deni