Taasisi mama ya ajira kwa upande wa walimu wa shule binafsi, Teachers Junction wamevunja ukimya kwa kuja na suluhisho lenye matokeo chanya, baada ya uwepo wa taarifa za kuzidiwa na idadi ya walimu wanaohitaji huduma na kuwalazimisha walimu wote kufika Dar es Salaam ili kujisajili.
Hayo, yamebainishwa hii leo Novemba 6, 2022 na Msimamizi wa mradi huo, Jactan Madowa na kuongeza kuwa, wameandaa utaratibu mpya wa ajira ambao ni suluhisho la ajira za Walimu kwa shule binafsi na kwamba sasa wanaweza kuingia kwenye mfumo na kufanya maombi kwa njia ya mtandao.
Amesema, “Tumefikiria juu ya walimu wa ngazi zote na namna ya kuwasadia, mfumo huu umeandaliwa ndani ya miezi sita, tunajiridhisha kuwa mwalimu akiweza kufanikisha kuvuka kwenye mfumo huu basi ni dhahiri yeye ni mwalimu mzuri.”
Kwa upande wake Msimamizi wa mfumu, Taasisi ya Teachers Junction, Madam Nah amesema kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo walimu wengi kutokuwa na elimu juu ya teknolojia na ufanyaji wa tathimini ya awali kwa njia ya mitandao.
Awali, Afisa Mradi wa Taasisi hiyo, Njama Salum (Mr. Njama), alisema, “Mfumo huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kupata aina ya Walimu wanaohitajika kwenye soko na unapatikana kwenye website yetu www.teachersjunction.co.tz ukimpa mwalimu uwezo wa kuingia na kujisajili akiwa sehemu yoyote nchini na Duniani kiujumla.”
Akieleza juu ya mfumo huo unavyofanya kazi, Mr. Njama amesema taarifa zinazoweza kuonekana ni matokeo ya mwalimu husika na si jina lake wala la shule na kwamba ataona matokeo ya chuo ili kuweka usiri wa taarifa na kuweka uhuru wa kazi na taarifa binafsi.