Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ lipo katika hatau za mwisho za kumuajiri na kumtangaza Kocha Mkuu mpya wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
‘Taifa Stars’ ambayo ipo kwenye mchakati wa kusaka nafasi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ imekua haina kocha tangu alipoondoka Kocha Hanour Janza aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, baada ya Kocha Kim Poulsen kurudishwa katika Timu za Taifa za Vijana.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Oscar Milambo amesema, wapo katika harua za mwisho kukamilisha mchakato wa kumpata Kocha huyo, kwa kufuata vigezo maalum ambavyo vitaiwezesha Taifa Stars kufanya vizuri kimataifa.
“Hivi sasa tupo kwenye mchakato wa kutafuta Kocha wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mchakato ambao unaendelea vizuri hadi sasa, muda sio mrefu tutautangazia umma tumefikia wapi na nani atapewa nafasi hiyo ya kukiongoza kikosi chetu.”
“Tunafahamu na tayari tuna ushahidi kwamba tumeshawahi kuwa na makocha, na nini pengine kilisababisha hatukufikia malengo tuliokuwanayo kama Shirikisho na kama nchi.”
“Kwa pamoja tunajaribu kufanya hesabu vizuri ili Kocha tutakayemtangaza tuwe tumejiridhisha kwamba hatutakutana na changamoto ambazo tumepitia siku za nyuma.” amesema Milambo
‘Taifa Stars’ itarejea dimbani mwezi Machi 2023 kupambana na Uganda katika mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Kundi F wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.
Timu nyingine zilizopangwa Kundi F ni Niger na Algeria ambazo tayari zimeshacheza dhidi ya Taifa Stars.