Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Elias Mwanjala, amebariki mpango wa klabu ya Simba kuongeza wachezaji watano wa kigeni wataotumika kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, itakayoanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mwanjala amebariki mpango huo, baada ya mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed ‘Mo’ kuzungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma lililopita na kueleza mpango wa kuwasilisha ombi la usajili huo TFF.
Mwanjala amesema ombi hilo litakapofika kwenye kamati yake ana uhakika litapitishwa kwa maslahi ya nchi, lakini akatoa angalizo juu ya wachezaji watakaosajiliwa kwa kusema hawatoweza kucheza hadi dirisha dogo litakapofunguliwa Disemba 15.
“Sina uhakika kama wameleta ombi hilo, ila wakileta wala hakuna kipingamizi,” alisema Mwanjala.
“Watawatumia kwenye Ligi ya Mabingwa na kwenye ligi ya ndani hawatacheza, wakitaka kuwatumia ndani watasubiri dirisha dogo (la usajili linaloanza Desemba 15 hadi Januari 15).”
Simba itaanzia ugenini kucheza na Plateau United ya Nigeria, Novemba 27, kabla ya kurudiana Desemba 4 jijini Dar es Salaam.