Shirikisho la soka nchini TFF limemtangaza mwamuzi Martin Saanya kuwa msimamizi wa sheria 17 za mchezo wa soka, wakati wa mpambano wa watani wa jadi Young Africans dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba, utakaochezwa Jumapili Machi 8, Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemtaja mwamuzi Saanya atachezesha mchezo huo, huku akisaidiwa na waamuzi sita, tofauti na idadi ya waamuzi wanne iliyozoeleka katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Saanya mkazi wa mkoani Morogoro, atasaidiwa msaidizi namba moja Mohamed Mkono (Tanga), msaidizi namba mbili akiwa ni Frank Komba wa Dar es Salaam.
Mwamuzi wa msaidizi Elly Sasii (Dar es Salaam na wengine wawili Abdallah Mwinyimkuu (Singida), Ramadhani Kayoko (Dar es Salaam). Mtathimini waamuzi Sudi Abdi (Arusha) na Kamishna wa mchezo Mohamed Mkweche (Dar es Salaam).
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa mchezo wa soka nchini kuchezeshwa na waamuzi sita, ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni katika mchezo wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation, uliofanyika katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni Mosi 2019.
Katika mchezo huo ambao Azam waliibuka na ushindi wa bao 1-0, mwamuzi wa kati alikuwa ni Hance Mabena aliyesaidiwa na washika kibendera, Mohamed Mkono na Ferdinand Chacha huku wa mezani akiwa ni Abubakar Mturo.
Waamuzi ambao walisimama nyuma ya magoli walikuwa ni Saanya na Florentina Zablon.
Mwamuzi Saanya amewahi kuchezesha mchezo wa Simba na Young Africans msimu wa 2012/13 uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, lakini siku chache baadaye alifungiwa, bada ya kubainia alishindwa kwenda sambamba na sheria 17.
Katika mchezo huo, Young Africans walitangulia kupata bao kupitia kwa mshambuliaji Amis Tambwe ambaye alidaiwa kuunawa mpira kabla ya kuutumbukiza nyavuni, hatua ambayo ilileta taharuki kwa mashabiki wa Simba SC na kufanya fujo, zilizopelekea kung’oa viti.
Lakini dakika za lala salama mshambuliaji Shiza Ramadhan Kchuya aliisawazishia Simba kwa mpira wa kona uliokwenda moja kwa moja nyavuni, huku mlinda mlango wa Young Africans kwa wakati huo Ally Mustafa akishindwa kufanya lolote.