Watazamaji wataingia bure katika mchezo wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes na vijana wenzao wa Morocco kesho Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam
Hayo yamesemwa na Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo ambapo amebainisha hilo leo kwenye mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya mchezo huo utakoanza Saa 10:00 jioni.
Ngorongoro iliyo chini ya kocha, Ammy Ninje itakuwa na mechi mbili za kirafiki na mbali na hiyo ya kesho, nyingine itafuatia Jumatano ya Machi 21, dhidi ya Msumbiji.
Aidha, mechi hizo ni maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la mataifa ta Afrika (AFCON U20) dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Machi 31 Uwanja wa Taifa na marudiano wiki mbili baadaye mjini Kinshasa.
Hata hivyo, Ngorongoro Heroes ipo kambini ikijiandaa na michezo hiyo miwili ya kirafiki na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Vijana Afrika wenye umri chini ya miaka 20 chini ya Ammy Ninje ambaye pia amewahi kuifundisha Kilimanjaro Stars.