Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limevitaka baadhi ya vyombo vya habari nchini kuacha mara moja kampeni za upotoshaji zenye lengo la kuwachafua viongozi wa juu wa shirikisho hilo.
TFF imeshtushwa na taarifa inayoendelea kutolewa kwenye gazeti moja la kila siku ikidai kuwa kuna ufisadi ndani ya shirikisho wakati madai hayo ni ya uongo na yenye lengo la kujenga mtazamo hasi dhidi ya shirikisho na viongozi wake.
Gazeti hilo la kila siku limetumia taarifa ya ukaguzi wa fedha iliyofanywa na wakaguzi kutoka TAC kujenga picha kuwa ni ushahidi tosha wa kuwepo kwa ufisadi ndani ya shirikisho.
Taarifa ya ukaguzi wa fedha ya TAC haikuwahi kuituhumu TFF kwa ufisadi. Taarifa ilibaini maeneo ya kiuhasibu ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya namna baadhi ya malipo yalivyofanyika (audit queries), na ufafanuzi ulitolewa kwa ufasaha na watendaji wa shirikisho na kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho.
Hata hivyo gazeti hilo ambalo limeonekana kuweka kando kabisa misingi ya uandishi wa habari, limechapisha taarifa bila hata kutoa nafasi kwa wanaotuhumiwa kujibu na kutoa ufafanuzi stahiki.
Rais na katibu mkuu wa shirikisho wanahudhuria mikutano ya CAF nje ya nchi wakati gazeti hilo likiendelea kuporomosha mlolongo wa tuhuma bila kutoa haki ya kusikilizwa kwa wanaoandikwa vibaya.
TFF inaliangalia suala hili kama kampeini chafu inayofanywa ili kushawishi matokeo ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Agasti mwaka huu.
Pia taarifa hii potofu inalenga kulihamisha taifa kutoka kwenye masuala ya msingi kama kuiunga mkono Serengeti Boys kwenye mashindano ya Afrika na kuanza kujadili masuala yanayohusiana na siasa za uchaguzi wa TFF.
TFF kwa sasa inatafakari hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya vyombo vya habari husika na inachukua nafasi hii kuvisihi vyombo vya habari kuacha mara moja kujihusisha na kampeni ya kuchafuana ambayo ni kinyume na misingi ya maadili ya uandishi wa habari.