Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Salum Madadi amesema hadi sasa hawajapokea taarifa zozote za Maafisa wa Klabu ya USM Alger kupuliziwa dawa kabla ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
USM Alger ilicheza dhidi ya Young Africans Jumapili (Mei 28) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku klabu hiyo kutoka nchini Algeria ikitoa taarifa za shutuma kwa wenyeji wao, wakidai kulikuwa na hujuma za chumba cha kubadilishia nguo cha Wachezaji kupuliziwa dawa kabla ya mchezo huo.
Madadi amesema TFF kama mwenyeji wa mchezo, hawafahamu lolote na wala hawajapokea taarifa zozote kuhusu shutuma hizo, ambazo jana Jumanne (Mei 30) zilisambazwa Katika mitandao ya Kijamii na USM Alger.
“Hatuna taarifa ya watu kupuliziwa dawa katika mechi ya Yanga na USM Alger. Na siwezi kulizungumzia suala hilo, labda Madaktari wa Yanga, Madaktari wa uwanjani na wenyeji USM Alger ndiyo wanaweza kulizungumzia zaidi.”
“Labda nizungumzie athari zilizojitokeza kutokana na wingi wa watu na kupelekea mwenzetu mmoja kupoteza maisha. Hii ni changamoto ya kutazama na maeneo mengine ya kiwanja, lazima tutafute namna ya kuepukana na majanga ya namna ile, tunamuomba Mungu atuepeshe mbali “ amesema Salum Madadi
Wakati TFF wakithibitisha kutopea taarifa zozote za kufanywa kwa hujuma za chumba cha kubadilishia cha USM Alger, Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ nalo halijatoa taarifa zozote za kupokea malalamiko ya klabu hiyo kutoka nchini Algeria.