Kufuatia Sakata la Usajili wa Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Tuisila Kisinda katika Klabu ya Young Africans, Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limetoa ufafanuzi.
Wadau wa soka hususan Mashabiki wa Young Africans wakiongozwa na aliyekua Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara wanadai Klabu yao imefanyiwa hujuma na TFF kwa kukataa usajili wa Kisinda aliyesajiliwa dakika chache kabla ya Dirisha la Usajili kufungwa mwishoni mwa mwezi Agosti.
TFF imetoa ufafanuzi wa sakata la Kiungo huyo kwa kusambaza taarifa katika Mitandao ya kijamii inayoeleza kanuni na taratibu za usajili wa Wachezaji wa Kigeni kwa Klabu za Tanzania Bara.
Taarifa hiyo ya TFF imetolewa mapema leo Jumatatu (Septemba 05) kufutia malalamiko ya Mashabiki na Wadau wengine wa Soka kuendelea kushika Hatamu katika Mitandao ya kijamii.
Taarifa ya TFF imeeleza: Usajili wa wachezaji wa kigeni, hasa kwa klabu ambazo timu zao zinacheza mashindano ya kimataifa ulishapitishwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji katika mazingira maalumu ilishughulikia haraka usajili wa wachezaji hao wa kigeni ili wawahi usajili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Wachezaji wote wa klabu hizo za Azam, Geita Gold, Simba, na Yanga walishapewa leseni zao kwa ajili ya msimu wa 2022/2023 ambazo pia ndizo zimetumika kuwaombea usajili kwa ajili ya mashindano ya CAF.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2022, klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12. Hivyo, klabu kutaka au kujaribu kusajili wachezaji zaidi ya idadi hiyo ni kwenda kinyume na kanuni.