Wakala wa misitu Tanzania – TFS, umeendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi za misitu na jamii, ambapo jumla ya hekta 296,881 za maeneo ya hifadhi zilitolewa kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji huku ikitoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa misitu na kuimarisha mipaka kwa kuweka vigingi na mabango, ili kuzuia uvamizi.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Jijini Dodoma, Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Misitu Tanzania, Dos Silayo amesema utatuzi wa migogoro kati ya hifadhi za misitu na Wananchi ni jukumu lao hivyo wataendelea kusimamia bila kuchoka.
Amesema, “hatutochoka kuwapatia elimu juu ya uhifadhi na pia jinsi ya usimamizi wa misitu, lakini pia tutaendelea kuimarisha mipaka kwa kuweka alama na vibao vinavyoelekeza ili tuendelee kuzuia huu uvamizi wa maeneo mbalimbali ya hifadhi.”
Hata hivyo amesema katika jitihada za kukabiliana na majanga ya moto kwenye hifadhi za misitu, Wakala umesafisha mipaka na njia za moto zenye urefu wa kilomita 5,416 huku Wananchi zaidi ya 19,170 kutoka vijiji 348 wakipatiwa elimu ya athari za moto na mbinu za kukabiliana nao.
“Vikosi vya kukabiliana na matukio ya moto vyenye jumla ya watu 365 viliimarishwa kwa kupewa mafunzo sambamba na kukarabati minara 21 ya kuangalizia moto katika mashamba ya miti, Wakala uliimarisha matumizi ya mitambo ya kuzimia moto na mfumo wa satelite wa kubaini matukio ya moto mapema, ili kuukabili kabla ya kuenea na kusababisha madhara zaidi,” alisema.