Klabu ya Leicester City imeripotiwa itapata wakati mgumu wa kuwauza kwa thamani zao halisi mastaa wao, James Maddison na Harvey Barnes dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Mastaa hao ni silaha kubwa za Leicester City ambao wameonyesha ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu licha ya timu yao kuwa na matokeo mabovu ndani ya uwanja.
Maddison amefunga mabao 10 na kuasisti tisa kwenye Ligi Kuu England, wakati Barnes amefunga 12 na kuasisti mara moja.
Licha ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Newcastle United Jumatatu (Mei 22), Leicester City bado ipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Leicester City watalazimika kushinda dhidi ya West Ham United katika mechi yao ya mwisho ya msimu Jumapili, huku wakiombea Everton washindwe kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Bournemouth uwanjani Goodison Park.
Chochote kitakachotokea Jumapili, Maddison atacheza mechi yake ya mwisho Leicester City hivyo miamba hiyo ya King Power italazimika kumpiga bei dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili asiondoke bure 2024. Maddison anathaminishwa kuwa Pauni 50 milioni.