Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi amefunguka kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, utakaowakutanisha na USMA.

Miamba hiyo ya Afrika itakutana Jumapili (Mei 28) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mjini Algiers Juni 03.

Kocha Nani amesema amefahamu ubora na udhaifu wa wapinzani wao baada ya kunasa faili la Waarabu hao, ambao wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam wakati wowote kuanzia sasa.

Nabi amesema tayari amewafuatilia wapinzani wake kwa njia ya video, na ameona ubora na udhaifu wao hao na kwa sasa anafanyia kazi mbinu zitakazomwezesha kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza nyumbani.

Nabi amesema michezo hiyo miwili ya fainali ni michezo ya matokeo zaidi hivyo anaandaa mbinu itakayowapa matokeo mazuri kwenye michezo yote ili kuweza kutwaa ubingwa wa Afria kwa mara ya kwanza.

“Mechi itakuwa ya ushindani mkubwa nalihitaji kuwafuatilia wapinzani wetu jinsi wanavyocheza wanapokuwa ugenini na nyumbani, nafurahi nimepata mikanda yao na bado tunaendelea kuifanyia kazi ingawa nimeona ubora na hata udhahifu wa wapinzani wetu, mechi hizi mbili ni mechi za matokeo zaidi,” amesema Nabi

Amesema moja ya kazi aliyoifanya ni kuwabaini wachezaji bora wa USM Alger na kuwapa mbinu wachezaji wake namna ya kukabiliana nao.

“Niwapongeze wachezaji wangu wamepambana na kufanikiwa kufika fainali ya michuano hii ya CAF, kazi iliyobaki kwetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye hatua hii, kuna mbinu ambazo tunazifanyia kazi na kuwapa wachezaji wetu, tunaamini tutafanya vizuri,” amesema Nabi

Amesema pia anashukuru viongozi wa Young Africans kwa kushirikiana naye bega kwa bega kuanzia mwanzo wa msimu kwa kufanya usajili mzuri na kuhakikisha wanapata mahitaji yote.

Nabi amesema tayari amewaambia wachezaji wake kuwa ni lazima wamalize kazi kwenye mchezo wao wa nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri kuelekea kwenye mchezo wa marudiano.

Amesema wamegundua mbinu wanazozitumia wapinzani wao kwenye michezo ya ugenini na ile wanayotumia kwenye michezo wanayokuwa nyumbani.

“Jambo kubwa ambalo kama benchi la ufundi tunalifanyia kazi kwa umuhimu mkubwa ni kutafuta namna ya kuhakikisha tunamaliza kazi kwenye mchezo wetu wa nyumbani, tupate ushindi mzuri ambao utatupa picha ya nini cha kufanya kuelekea kwenye mchezo wa marudiano,” amesema Nabi

Young Africans itahitaji ushindi mzuri kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza hapa nyumbani kabla ya kuelekea jijini Alger nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Granit Xhaka: Mikel Arteta anatosha Arsenal
Mtaala mpya wa Elimu kuijumuisha lugha ya alama