Tanzania, imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism Expo), yanayofanyika nchini humo kuanzia Septemba 22 – 25, 2022 kuzindua filamu ya “The Royal Tour” iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kijapan.
Katika hotuba yake, wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Septemba 22, 2022, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda aliwasihi washiriki kuiangalia “The Royal Tour” ambayo inavionesha vivutio vya Tanzania ikiwemo hifadhi za taifa za wanayamapori, milima na fukwe.
Amebainisha kuwa, tukio hilo la uzinduzi wa filamu limefanyika katika kipindi kizuri ambapo dunia inaanza kufunguka kutokana na masharti ya kusafiri baina ya nchi kupunguzwa, baada ya kupungua kwa mambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona Duniani.
Balozi Luvanda amesema, “Ni matumaini yangu kuwa washiriki wa maonesho haya na wageni wengine, mtapanga safari za kutembelea Tanzania kujionea wenyewe vivutio vya utalii mnavyovishuhudia katika filamu hii na kwenye banda la Tanzania lililopo kwenye Maonesho haya.”
Tanzania, imejipanga kutangaza vivutio vya utalii kwa kutumia majukwaa mbalimbali yakiwemo kama hayo ya maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan, ambayo yanashirikisha wadau wengi wa utalii kutoka duniani kote.
Wadau wa Tanzania, wanaoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).